Rais Magufuli: Watakaofanya maandamano 'watasimulia' baba zao
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amevionya vyama vya siasa na wananchi ambao wamepanga kufanya maandamo siku za hivi karibuni kwa mujibu wa taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa mitandaoni.
Rais Magufuli amesema hayo wakati akizindua Tawi la CRDB-Bank, Chato mkoani Geita na kuwataka waliojiandaa kutekeleza mpango waache mara mora vinginevyo watashughulikiwa.
Rais Magufuli amsema: “Nchi hii ni ya amani, ndiyo maana uvunjifu wa amani ulipoanza kutokea kule Kibiti tuliamua kuufuta mara moja. Kuna watu wanadhani tunafanya siasa kila wakati, kama wametumwa na baba zao kuandamana, watawasimulia vizuri.
Rais wa Tanzania amebainisha kwamba, “Wapo Watanzania wachache ambao hawapendi kuambiwa ukweli, wanapenda kuambiwa maneno matamu. Mimi niliomba kura kwa wananchi wangu kwa kusema ukweli, nitaendelea kusisitiza ukweli daima.
Aidha Rais Magufuli amesema kama ninavyyomnukuu: "Wapo watu ambao wameshindwa kufanya siasa za kweli, wangependa kila siku tuko barabarani tunaandamana. Watu wao wanahamia huku, wao wanataka wabaki wanaandamana kule. Nitasema ngoja waandamane wataniona. Kama kuna baba zao wanawatuma, watakwenda kuwasimulia vizuri."
Wakati huo huo, jeshi la polisi nchini Tanzania limetoa onyo kali na kusema kuwa, atayeandamana asije kulilaumu jershi hilo la polisi. Jeshi la Polisi limetoa onyo kwa kikundi kinachohamasisha maandamano kupitia mtandao wa Telegram na kusema litafanya kila liwezekanalo kisheria kukizuia.
Hayao yanajiri huku serikali ya Rais Magufuli ikiendelea kulaumiwa na vyama vya upinzani na asasi za kutetea haki za binadamu kutokana na kupiga marufuku maandamano hatua ambayo inatajwa kuwa ni kukandamiza demokrasia.