Uchaguzi wa Rais Sierra Leone waingia duru ya pili
Matokeo ya uchaguzi mkuu nchini Sierra Leone yameonesha kwamba, hakuna mgombea aliyefanikiwa kupata ushindi mutlaki na kwa msingi huo uchaguzi huo umeingia duru ya pili.
Matokeo hayo yameonesha kuwa, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Sierra Leone, Samura Kamara wa chama tawala cha All People’s Congress na mpinzani wake wa chama cha Sierra Leone People’s, Julius Maada Bio kila mmoja amepata karibu asilimia 43 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa Jumatano iliyopita.
Zaidi ya Wasierra Leone milioni tatu waliokamilisha masharti walikwenda kwenye masanduku ya kupigia kura kuchagua rais wa nchi na wawakilishi wao katika Bunge la nchi hiyo. Wagombea 16 walichuana kuwania kiti cha rais ingawa ushindani mkubwa zaidi ulikuwa baina ya mgembea wa chama tawala, Samura Kamara na yule wa chama cha Sierra Leone People’s, Julius Maada Bio.
Kwa mujibu wa Katiba ya Sierra Leone, Rais anayemaliza muda wake, Ernest Bai Koroma hawezi kugombea tena kiti hicho kwa mara ya tatu baada ya kuongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili. Kabla ya kufanyika uchaguzi huo ilitabiriwa kwamba, kuna uwezekano mkubwa ukaingia duru ya pili kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kugombea nafasi hiyo.
Tangu baada ya kupata uhuru Sierra Leone imekuwa ikiongozwa na moja kati ya vyama viwili vikuu hasimu yaani chama tawala cha All People’s Congress na kile cha Sierra Leone People’s Party ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani. Ripoti zilizotolewa jana jioni zilisema kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Sierra Leone imelazimika kuhesabu tena kura za uchaguzi mkuu nchini humo katika majimbo 83 baada ya kuwasilishwa malalamiko ya kukiukwa taratibu za uchaguzi katika majimbo hayo. Pamoja na hayo wataalamu wanasema kuwa, zezi hilo la kuhesabiwa tena matokeo ya kura za uchaguzi mkuu wa Sierra Leone katika baadhi ya majimbo halitakuwa na taathira ya maana katika jumla ya matokeo ya uchaguzi huo.
Uchaguzi mkuu wa jana nchini Sierra Leone ulifanyika huku nchi hiyo ikizongwa na matatizo mengi ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha ukosefu wa ajira baina ya raia nchini humo kimeongezeka na kufikia asilimia 70, na Wasierra Leone wengi wanatarajia kuona rais ajaye wa nchi hiyo akiboresha hali ya uchumi na maisha yao. Takwimu zinaonesha kuwa miongoni mwa sababu za matatizo hayo ya kiuchumi ni kuporomoka kwa bei ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi hiyo.
Changamoto nyingine zinazomkabili kiongozi ajaye wa Sierra Leone ni huduma duni za afya na ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma. Ugonjwa wa Ebola ulioiathiri zaidi Sierra Leone uliua zaidi ya watu elfu nne na idadi kubwa ya familia za wahanga wa ugonjwa huo zinakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi licha ya kupita miaka miwili sasa tangu janga hilo litangazwe kumalizika rasmi nchini humo. Manusura wengi wa ugonjwa huo pia wanailaumu serikali ya Free Town kwamba imeshindwa kuwasaidia kujikwamua na athari mbaya za miaka kadhaa ya jinamizi hilo. Yusuf Kaba ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Manusura wa Ebola anasema: Ni haki yetu kupata huduma nzuri za afya na maisha bora, lakini serikali imepuuza masuala hayo kutokana na uongozi mbaya na usiofaa."
Kinachosubiriwa sasa na Wasierra Leone ni kuona rais ajaye atafanya nini kuboresha hali ya kiuchumi na kijamiii ya nchi hiyo tajiri kwa madini na maliasili ya magharibi mwa Afrika.