Mar 13, 2018 03:07 UTC
  • Nigeria kuzungumza na Boko Haram kuhusu kuachiwa huru wasichana 110 waliotekwa

Serikali ya Nigeria imesema inapanga kufanya mazungumzo na kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram juu ya kuachiwa huru makumi ya wasichana wa shule waliotekwa na wanamgambo hao mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu ya Rais Muhammadu Buhari imesema serikali inafadhilisha kutumia njia ya mazungumzo kunusuru maisha ya wanafunzi hao wa kike, badala ya chaguo la kijeshi.

Takriban wasichana 110 waliweka baada ya kundi la kigaidi la Boko Haram kushambulia shule moja katika kijiji kilichoko mjini Dapchi, huko kaskazini mashariki mwa jimbo la Yobo nchini Nigeria Februari 19.

Itakumbukwa kuwa, kati ya wasichana 270 wa Shule ya Chibok waliotekwa na genge hilo mwaka 2014, 170 tayari wamekwishaachiwa huru baada ya kile vyombo vya usalama vinasema ni kuwalipia kikomboleo. Wengine zaidi ya 100 wangali wanashikiliwa mateka na magaidi hao.

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Chibok walioachiwa huru na Boko Haram

Tokea kundi la kigaidi la Boko Haram lianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu 20 elfu wameuawa. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa Boko Haram.

Aidha wigo wa harakati na mashambulio ya Boko Haram umepanuka hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.

Tags