Mtandao wa wanafunzi Tanzania: Hatuamini uchunguzi uliofanywa na polisi kuhusu Nondo
Mtandao wa wanafunzi nchini Tanzania (TSNP) umetoa taarifa ukisema kuwa, habari walizo nazo kuhusu kile kilichomsibu mwanafunzi mwenzao, Abdul Nondo, zinakinzana na zile zilizotolewa jana na jeshi la polisi nchini humo hasa baada ya kufanya uchunguzi.
Taarifa za kupotea kwa Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka hapo tarehe sita Machi mwaka huu, baada ya mwanafunzi huyo (Nondo) kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa, usalama wake uko hatarini. Msemaji wa TSNP Helllen Sisya amesema bado wanasubiri kauli na Nondo mwenyewe ili kujua nini kilitokea na sio ripoti pekee ya polisi. “Sisi bado hatuamini uchunguzi uliofanywa na polisi kwa kuwa hatujamsikia Nondo akiongea na kile tulichoelezwa na polisi mkoani Iringa na hiki tulichokisikia jana kwa polisi Dar es Salaam haviendani”, alisema Sisya.
Mtandao wa Wanafunzi Tanzania ambao ulitoa taarifa kwa umma kuhusu kupotea kwa Abdul Nondo, umesisitiza kuwa, haukubaliani kabisa na taarifa hiyo ya polisi kwa kudai kuwa inakanganya. Taarifa hiyo imefafanua kuwa, polisi wanadai kuwa alipatikana akiendelea na shughuli zake za kawaida alipoenda kumtembelea rafiki yake na wakati wao walipata taarifa kutoka kwa jeshi la polisi mkoa wa Iringa kuwa Nondo alifika kituoni hapo akiwa hajitambui. Mapema jana jeshi la polisi nchini Tanzania lilizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam, Abdul Nondo aliyedaiwa kupotea katika mazingira ya kutekwa ulikuwa uzushi.
Kamanda wa Polisi, Lazaro Mambosasa alidai kuwa taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na kuzua taharuki hapo tarehe sita ya mwezi huu kwa madai kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana si za kweli kwa kuwa uchunguzi wa jeshi la polisi umebaini kwamba, mwanafunzi huyo alikutwa akiendelea na shughuli zake za kawaida na wala hakutekwa kama ilivyodaiwa kuwa ametekwa nyara.