Rais wa Botswana asema Trump anashajiisha ujangili, magendo ya vipusa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41843-rais_wa_botswana_asema_trump_anashajiisha_ujangili_magendo_ya_vipusa
Rais Ian Khama wa Botswana amesema Rais Donald Trump wa Marekani anaunga mkono na kushajiisha ujangili barani Afrika, kufuatia hatua yake ya hivi karibuni ya kuangalia upya marufuku ya vipusa na bidhaa nyingine zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 18, 2018 13:01 UTC
  • Rais wa Botswana asema Trump anashajiisha ujangili, magendo ya vipusa

Rais Ian Khama wa Botswana amesema Rais Donald Trump wa Marekani anaunga mkono na kushajiisha ujangili barani Afrika, kufuatia hatua yake ya hivi karibuni ya kuangalia upya marufuku ya vipusa na bidhaa nyingine zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu.

Khama ameyesema hayo katika mkutano wa Afrika wa kuhamasisha kuhifadhiwa ndovu uliofanyika nchini Botswana na kuongeza kuwa, hatua ya Washington ya kuondoa marufuku hiyo kwa baadhi ya nchi za Afrika itapelekea kuongezeka harakati za ujangili katika misitu ya bara hilo.

Rais wa Botswana amesema, "Nataka kuchukua fursa hii kulaani vikali hatua ya utawala wa Trump ya mnamo Machi Mosi mwaka huu, ambapo ulisema utatoa kibali kwa nchi 6 za Afrika, kuruhusiwa kutuma nchini Marekani vipusa na bidhaa mbali mbali kama vile tuzo zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu. Hatua hiyo itadunisha jitihada zetu za kupambana na ujangili na magendo ya pembe za ndovu."

Rais Ian Khama wa Botswana

Amesisitiza kuwa, sheria za Botswana ziko wazi na katu hawawezi kuruhusu ujangili kushamiri na kusababisha hatari ya kutoweka kwa ndovu katika misitu na mbuga za nchi hiyo. Amesema kuangamia kwa kizazi cha ndovu kutakuwa na taathira hasi kwa utalii wa nchi na kutoweka kwa moja ya turathi zenye thamani kubwa.

Nchi za Afrika zilizoruhusiwa kuiuzia Marekani ngozi na pembe za ndovu ni Botswana yenyewe, Tanzania, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Namibia.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, bara la Afrika lilikuwa na ndovu milioni 13 mwaka 1979, lakini kushadidi magendo ya vipusa kumesababisha idadi hiyo kupungua hadi laki 4 hivi.