Mar 25, 2018 02:21 UTC
  • Jeshi la Chad lapambana na magaidi wa Boko Haram

Duru za kijeshi za Chad zimetangaza habari ya kutokea mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na magaidi wa Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad.

Duru hizo zimesema kuwa, magaidi 20 wa Boko Haram wameuawa katika mapigano hayo kama ambavyo mwanajeshi mmoja wa serikali ameuawa na wengine watano kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa duru hizo za kijeshi, katika mapigano hayo, jeshi la Chad limefanikiwa kukamata silaha nyingi kutoka kwa genge la Boko Haram na kusambaratisha maficho yao.

Miongoni mwa jinai zinazofanywa na magaidi ya Boko Haram ni kuteka wasichana na baadaye kuwapiga mnada kama bidhaa

 

Jeshi la Chad aidha limesema kuwa, wanajeshi wawili wa nchi hiyo waliuawa mwezi mmoja uliopita katika shambulizi la kuvizia lililofanywa na magaidi wa Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad.

Mashambulio ya Boko Haram yalianza mwaka 2009 nchini Nigeria kwa madai ya kupinga elimu za nchi za Magharibi. Mwaka 2015 kundi hilo lilipanua wigo wa mashambulizi yake hadi katika nchi jirani na Nigeria yaani Cameroon, Chad na Niger.

Nchi hizo nne zimeunda jeshi la pamoja la kupambana na magaidi wa Boko Haram lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kuwamaliza magaidi hao.

Tangu mwaka 2009 hadi hivi sasa kundi hilo la wakufurishaji limeshapelekea zaidi ya watu elfu

20 kuuawa katika nchi hizo nne za Nigeria, Niger, Cameroon na Chad, na zaidi ya milioni mbili wengine kuwa wakimbizi.

Tags