Hatimaye Abdul Nondo aachiliwa huru na mahakama ya Tanzania kwa dhamana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42218-hatimaye_abdul_nondo_aachiliwa_huru_na_mahakama_ya_tanzania_kwa_dhamana
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa Jumatatu ya leo, imemuachilia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kwa dhamana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 26, 2018 04:17 UTC
  • Hatimaye Abdul Nondo aachiliwa huru na mahakama ya Tanzania kwa dhamana

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa Jumatatu ya leo, imemuachilia huru Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini Tanzania (TSNP), Abdul Nondo kwa dhamana.

Habari zinasema kuwa, Nondo ameachiliwa huru kwa dhamana ya Shilingi milioni tano na mali isiyohamishika. Abdul Nondo amepewa dhamana hiyo mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia anayeendesha kesi hiyo baada ya mtuhumiwa kukamilisha taratibu zote za dhamana.

Abdul Nondo, alipokuwa mahakamani

Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita, Nondo alinyimwa dhamana baada ya upande wa mashtaka ambao ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kudai kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwa sababu za usalama wake. Nondo anayesimamiwa kesi yake na wakili Jebra Kambole anatuhumiwa kwa makosa mawili ambayo la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni tarehe saba Machi mwaka huu akiwa Ubungo na kusambaza ujumbe huo katika kutumia mtandao wa kijamii wa WhatsApp kwamba alikuwa hatarini.

Alipofikishwa polisi Iringa baada ya kupatikana

Ama kosa la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga, Iringa alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi mjini hapo kwamba, alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga. Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 10 Aprili mwaka huu.