Indhari ya Amnesty International kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu Mauritania
Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetahadharisha kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Mauritania na kulaani kukandamizwa watetezi wa haki za binadamu nchini humo.
Francois Patuel mtaalamu na mtafiti wa Magharibi mwa Afrika wa shirika la Amnesty International amesema kuwa leo hii kunashuhudiwa viashria vya utumwa na ubaguzi huko Mauritania na kwamba watu elfu 43 wanaishi katika mazingira kama ya watumwa.
Patuel ameongeza kuwa, ukandamizaji dhidi ya raia unafanyika nchini Mauritania kwa njia mbalimbali kama kuwatia watu mbaroni kiholela, utesaji, kukandamiza maandamano ya amani na kuzuia shughuli za taasisi mbalimbali bila ya vibali vya serikali.
Shirika la Amnesty International limesisitiza udharura wa kuachiwa huru watetezi wa haki za binadamu walioko katika jela za Mauritania na kuitaka serikali ya nchi hiyo kuzifanyia marekebisho sheria zinazopelekea kukandamizwa na kuteswa watetezi wa haki za binadamu. Amnesty International pia imeitaka serikali ya Mauritania kuacha kupasisha sheria na adhabu kali.
Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa, watetezi wa haki za binadamu 268 wametiwa mbaroni nchini Mauritania tangu mwaka 2014 na kwamba 17 miongoni mwao wamekabiliwa na mateso.