Viongozi wa upinzani Tanzania wakamatwa; wapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42284-viongozi_wa_upinzani_tanzania_wakamatwa_wapandishwa_kizimbani_na_kusomewa_mashtaka
Viongozi kadhaa wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania wamepandishwa kizimbani mchana wa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline, uasi, kuhamasisha chuki kati ya wanajamii na kuchochea ghasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 27, 2018 12:53 UTC
  • Viongozi wa upinzani Tanzania wakamatwa; wapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka

Viongozi kadhaa wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania wamepandishwa kizimbani mchana wa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka manane yakiwemo ya kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline, uasi, kuhamasisha chuki kati ya wanajamii na kuchochea ghasia.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni baada ya viongozi hao kuzuiliwa katika makao makuu ya polisi jijini hapo wakati walipokuwa wameripoti asubuhi kama inavyowataka dhamana yao. Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka hayo na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri. Aidha kosa la nane, linamkabili mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambalo ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai. Viongozi wa Chadema waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Mwenyekiti Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Vincent Mashinji, Manaibu Katibu Mkuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Esther Matiko na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Hii ni katika hali ambayo viongozi wengine wa Chadema John Heche na Halima Mdee hawakuripoti polisi kwa ajili ya kuhojiwa na hivyo hawakufikishwa mahakamani. Wakili wa viongozi hao wa Chadema, Frederick Kihwelo amesema kuwa shakhsia hao wa upinzani wamenyimwa dhamana kwa kile kilichodaiwa mahakamani kwamba kila wanapotakiwa kuripoti polisi, baadhi yao huwa wanashindwa kutokea. Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana tuhuma hizo dhidi yao ambapo wakili wa serikali amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali. Kadhalika, Nchimbi amewasilisha maombi kwa mahakama hiyo ili washtakiwa wanyimwe dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania. Itakumbukwa kuwa, Februari 20 mwaka huu, polisi kanda ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema, ikiwa ni siku chache baada ya kujiri tukio la kuuawa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini hapo tarehe 16 ya mwezi huo.

Akwilina Akwilini, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16

Mwanafunzi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya basi la abiria la daladala eneo la Kinondoni wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.