Saudia yalaumiwa kwa utumwa wanaofanyiwa wanawake wa Mauritania
Mashirika ya haki za binadamu yamelaumu vikali vitendo viovu wanavyofanyiwa wanawake wa Mauritania nchini Saudi Arabia na kusema kuwa wasichana wadogo wanaofanya kazi nchini Saudia wanageuzwa watumwa.
Mashirika hayo ya haki za binadamu yamesema kuwa, wasichana wa kike raia wa Mauritania wanarubuniwa kuwa na maisha mazuri na kazi za heshima huko Saudi Arabia lakini wanapofika wanafanywa watumwa na milki za waajiri wao.
Mashirika hayo yamelaani pia vitendo viovu kama vya kunyimwa chakula, kupigwa na kutumiwa vibaya kijinsia wasichana hao huko Saudi Arabia.
Hivi sasa mamia ya wasichana wa Mauritania wanajiandikisha kwa ajili ya kutumwa kufanya kazi nchini Saudi Arabia. Hivyo asasi za kiraia zisizo za kiserikali ambazo zinapigania haki za binadamu zimelalamikia vikali suala hilo na kusema kuwa hakuna uhalali wowote wa kisheria wa kuendelea kutumwa nchini Saudia wasichana hao.
Mwaka jana 2017 serikali ya Mauritania ilifikia makubaliano na Saudi Arabia ya kutuma watu 15 elfu nchini humo kwa ajili ya kufanya kazi. Hata hivyo hatua hiyo ya serikali ya Nouakchott inaendelea kulaaniwa na mashirika ya haki za binadamu ambayo yanazilaumu pia taasisi zinazowatuma wasichana hao kwenda kufanya kazi katika nchi ambayo wanageuzwa kuwa watumwa.