Rais John Magufuli: Polisi Tanzania hawakuajiriwa kufyeka mashamba ya bangi (sauti)
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42774-rais_john_magufuli_polisi_tanzania_hawakuajiriwa_kufyeka_mashamba_ya_bangi_(sauti)
Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, hakuna kitu kinachomkera kama askari polisi kwenda kufyeka mashamba ya bangi yaliyokamatwa na polisi hao akisisitiza kwamba polisi hawakuajiriwa kwa ajili ya kazi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 07, 2018 11:52 UTC

Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, hakuna kitu kinachomkera kama askari polisi kwenda kufyeka mashamba ya bangi yaliyokamatwa na polisi hao akisisitiza kwamba polisi hawakuajiriwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Rais Magufuli amewataka makamanda wa jeshi la polisi kutowaamuru maafisa wao kukata na kufyeka mashamba hayo na ameongeza kwa kusema: "Niwashauri tu kwamba, tumieni njia za kiintelijensia, mtawashika tu, kama shamba lipo karibu na kijiji, kamata kijiji kizima, wazee, vijana, wanawake hata na watoto, ndio wakafyeke hilo shamba la bangi." Amesema Rais Magufuli.

Polisi Tanzania wakifyeka shamba la bangi hivi karibuni

Ameongeza kuwa, mashamba hayo yanatakiwa kutumiwa katika kuwanasa na kuwabaini wamiliki wake, kuwakamata na kuwashughulikia ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria. Magufuli ameyasema hayo leo wakati akiwahutubia wakazi wa mkoa wa Arusha katika uwanja wa Amri Abeid baada ya kuzindua kituo cha polisi na nyumba za polisi mjini humo.

Amesema: “Nasema askari wasiende kufyeka bangi, hawakuajiriwa kufyeka bangi, usiwatume askari wako kufyeka bangi, wataumwa na nyoka bure, wamevaa uniform nzuri, msidhalilishe jeshi kwa kufyeka bangi, mimi nisingefyeka bangi wakati watu wa kufyeka wapo." 

Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania ambaye hivi karibuni naye alishiriki kuchoma moto shamba la bangi

Aidha amesema kwamba, amewahi kumuona mmoja wa mawaziri wake akifyeka na kuchoma moto shamba la bangi hivi karibuni na pia akamuona RPC wa Dodoma naye akifyeka shamba la bangi kwa kushirikiana na askari wake ambapo baada ya kuchoka, alisema watarudi tena kulimalizia siku ijayo, suala ambalo amesema lilimshangaza sana binafsi kama rais. Katika upande mwingine Rais John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la polisi na vyombo vingine vya Usalama nchini Tanzania kuendelea kuimarisha hali ya amani nchini humo kwa kuwatumikia Watanzania katika maendeleo ya taifa.