Rais wa Algeria ajitokeza hadharani baada ya miaka mingi
Rais Abdelazizi Bouteflika wa Algeria amejitokeza hadharani baada ya miaka mingi kutoonekana kadamnasi kutokana na hali yake mbaya ya kiafya.
Taarifa zinasema Bouteflika alijitokeza hadharani katika tukio nadra Jumatatu wakati wa kuzinduliwa msikiti na kupanuliwa reli ya chini ya ardhi katika mji mkuu Algiers.
Bouteflika alionekana akiwa katika kiti cha magurudumu au wheelchair wakati wa kufungua Msikiti wa Ketchaoua uliokarabatiwa na baada ya hapo akaelekea eneo jingine mjini Algiers na kufungua kituo kipya cha treni ya chini ya ardhi au metro.
Inasemekana kuwa kujitokeza kwake hadharani kunazipa nguvu tetesi kuwa, rais huyo mwenye umri wa miaka 81 huenda akagombea tena kwa mara ya tano katika ujao wa urais. Bouteflika alichaguliwa kwa muhula wa nne mwaka 2014, mwaka moja baada ya kupata kiharusi kilichopelekea alazwe hospitalini mjini Paris kwa zaidi ya miezi miwili.
Kiongozi huyo ambaye ameitawala Algeria kwa karibu miongo miwili ni nadra kujitokeza hadharani huku kukiwa na uvumi kuhusu hali yake ya kiafya.
Rais Abdelazizi Bouteflika amejitokeza hadharani siku moja baada ya katibu mkuu wa chama cha National Liberation Front (FLN), DJamel Ould Abbes, kumtaka agombee urais kwa mara nyingine katika uchaguzi wa mwaka 2019.