Waziri Mkuu Tanzania: Ni kweli kuna changamoto za muungano
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameelezea kuwepo changamoto katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kadhalika Waziri Mkuu Majaliwa amsema kuwa, hajaridhishwa na mjadala wa masuala yanayohusiana na muungano bungeni, lakini akasema kuwa ulikuwa na hoja. Majaliwa aliyasema hayo wakati akifanya majumuisho ya bajeti ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19 bungeni Jumanne ya jana Aprili 10. “Ni mgogoro wa mtu na mtu na ni mambo ambayo hayana tija. Natambua muungano unaendelea vizuri lakini kuna changamoto.”
Amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Aidha Majaliwa amesema licha ya changamoto za muungano kuwepo, viongozi wa pande zote wameapa kuulinda huku akisisitiza kuwa kwa namna ambavyo mjadala uliendelea jana, haukuwa na maana. “Hatuzuii mbunge kuuliza swali au kujenga hoja bali majibizano yasiyo na afya hayatakiwi.” Amesema. Inafaa kuashiria kuwa, juzi wabunge wa chama cha Wananchi CUF walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuzuia mjadala wa Muungano. Kabla ya hapo mbunge wa viti Maalumu wa chama cha Demokrasia na Maendelea (CHADEMA) Mariam Msabaha alisema kuwa serikali ya Muungano inaiminya Zanzibar na hivyo kushindwa kujitangaza kimataifa.