Mafuriko yashtadi Tanzania, watu tisa waripotiwa kufariki dunia huku mvua zikiendelea kunyesha
Jeshi la polisi nchini Tanzania limetangaza kuwa hadi sasa watu tisa wameripotiwa kufariki dunia jijini Dar es Salaam kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua kali zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti.
Kamanda wa Polisi wa kanda maalumu jijini Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa mbali na watu tisa kufariki dunia, wengine kadhaa pia wamejeruhiwa. Mkuu wa mkowa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaomba wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari na kuondoka maeneo hayo na ametahadharisha kwamba, kuna uwezekano wa kunyesha mvua kali zaidi katika siku zijazo.
Mbali na Dar es Salaam, mafuriko hayo yameshuhudiwa katika maeneo mengine mengi ya Tanzania kama Zanzibar, Morogoro, mkoa wa Pwani, Arusha na kadhalika huku kukiwepo ripoti za hasara za roho na mali. Katika hali hiyo polisi mkoani Arusha imetangaza kuwa kwa akali watu wawili walipoteza maisha Jumapili ya jana kutokana na mvua hizo. Habari kutoka Dar es Salaam na Zanzibar zinaarifu kusimama shughuli za wakazi wa maeneo hayo kutokana na njia kufurika maji na kushindwa kupitika. Kadhalika mamia ya wakazi wa jiji hilo wameripotiwa kupoteza makazi yao kutokana na nyumba zao kujaa maji au kusombwa na maji. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Mkurugenzi wa TMA, Agnes Kijazi amesema: "Mvua zitaendelea kunyesha na hii inatokana na kipindi hiki kuwa na mvua kubwa kuliko wastani."
Hii sio mara ya kwanza kwa mvua kusababisha madhara nchini Tanzania na miundombinu dhaifu inatajwa kuwa chanzo kikuu cha matatizo hayo.