UNICEF: Watoto wengi waliokuwa jeshini Sudan Kusini wameachiliwa huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43372-unicef_watoto_wengi_waliokuwa_jeshini_sudan_kusini_wameachiliwa_huru
Watoto zaidi ya 200 waliokuwa wamesajiliwa kama wanajeshi katika makundi ya wapiganaji nchini Sudan Kusini wameachiliwa huru.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 20, 2018 07:21 UTC
  • UNICEF: Watoto wengi waliokuwa jeshini Sudan Kusini wameachiliwa huru

Watoto zaidi ya 200 waliokuwa wamesajiliwa kama wanajeshi katika makundi ya wapiganaji nchini Sudan Kusini wameachiliwa huru.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya watoto UNICEF, watoto hao walikuwa kwenye Jeshi la kundi la waasi la National Liberation Movement (SSNLM) ambalo mwaka 2016 lilitia saini makubaliano ya amani na serikali.

UNICEF nchini Sudani Kusin inasema inahitaji dola za Marekani milioni 45 kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za kuwaachia watoto kwenye vikosi na kuwakutanisha watoto 19,000 na familia zao miaka mitatu ijayo.

Umoja wa Mataifa unasema kuna takriban watoto 19,000 ambao wanatumikia majeshi ya serikali na makundi ya waasi na wanamgambo nchini Sudan Kusini.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Kwa mujibu wa chanzo kutoka UNICEF, watoto wakirejea nyumbani, wazazi wao watapatiwa msaada wa chakula kwa ajili ya kusaidia kupambana na upungufu wa chakula.

Kulingana na taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto, sasa jitihada zinafanyika kuhakikisha watoto wengine wanaachiwa siku za usoni.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.