Mfalme wa Swaziland abadilisha jina la nchi yake kuwa eSwatini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43380-mfalme_wa_swaziland_abadilisha_jina_la_nchi_yake_kuwa_eswatini
Mfalme wa Swaziliand, Mswati wa Tatu, ametangza kubadilisha jina la nchi yake ambayo sasa itajulikana kama Ufalme wa eSwatini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 20, 2018 07:31 UTC
  • Mfalme wa Swaziland abadilisha jina la nchi yake kuwa eSwatini

Mfalme wa Swaziliand, Mswati wa Tatu, ametangza kubadilisha jina la nchi yake ambayo sasa itajulikana kama Ufalme wa eSwatini.

Alitangaza uamuzi huo wa ghafla katika sherehe za mwaka wa 50 wa uhuru wa Uswazi pamoja na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwake ambapo pia ametimiza miaka 50.

Katika mikutano kadhaa ya hadhara Mfalme Mswati wa Tatu amekuwa akiitaja nchi yake kwa jina la eSwatini, kwa maana ya  'ardhi au nchi ya Waswazi' kwa lugha ya Kiswati au Kiswazi. Mfalme huyo alitumia jina hilo la eSwatini katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka uliopita wa 2017.

Swaziland sasa itajulikana kama eSwatini

Mfalme Mswati amesema mabadiliko hayo yatapelekea nchi yake irejee katika jina lake asili kabla ya zama za ukoloni wa Muingereza. Nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru wake mwaka 1968.

Aidha mfalme huyo amesema jina hilo jipya pia litapelekea kutatuliwa tatizo la kimataifa ambapo watu wengi wamekuwa wakiitaja nchi hiyo kuwa ni Switzerland, nchi ya Ulaya Magharibi.