eSwatini (Swaziland) kutokata uhusiano na Taiwan licha ya mashinikizo ya China
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45288-eswatini_(swaziland)_kutokata_uhusiano_na_taiwan_licha_ya_mashinikizo_ya_china
Jamhuri ya eSwatini (Swaziland) imesisitiza kuwa haitakata uhusiano wake wa kidiplomasia na Taiwan licha ya mashinikizo ya kila upande kutoka China.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 02, 2018 04:08 UTC
  • eSwatini (Swaziland) kutokata uhusiano na Taiwan licha ya mashinikizo ya China

Jamhuri ya eSwatini (Swaziland) imesisitiza kuwa haitakata uhusiano wake wa kidiplomasia na Taiwan licha ya mashinikizo ya kila upande kutoka China.

Percy Simelane, Msemaji wa serikali ya eSwatini aliliambia shirika la habari la Reuters jana Ijumaa kuwa, "Hatujabadili msimamo kuhusu uhusiano wetu na Taiwan, na yule anayeeneza uvumi kuwa tunataka kukata uhusiano wa Taiwan anafaa kuchukuliwa kama msambazaji wa habari bandia."

Mapema jana, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema inatumai kuwa eSwatini itaghairi msimamo wake na kukata uhusiano na Taiwan kabla ya mwanzoni mwa Agosti, ambapo Beijing inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano na viongozi wa nchi za Afrika.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, China na Burkina Faso zilianzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuvunja uhusiano wake na Taiwan, ukiwa ni ushindi mwingine kwa Beijing inayoendelea kutoa mashinikizo kwa serikali ya Taipei.

Bendera za China na Taiwan

Kufuatia hatua hiyo, sasa Taiwan imebaki kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi moja tu ya Kiafrika, ambayo ni Jamhuri ya eSwatini (Swaziland).

Kwa ujumla kisiwa hicho kwa sasa kina uhusiano na nchi 18 tu duniani, baada ya Jamhuri ya Dominican, Sao Tome and Principe na Panama kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na kisiwa hicho.

China inaitambua Taiwan ambayo mwaka 1949 ilijitenga na nchi hiyo baada ya vita vya ndani, kuwa ni sehemu ya ardhi yake na kwamba haina haki ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na nchi nyingine yoyote ile.