AU yaitaka eSwatini itengue marufuku ya vyama vya siasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48330-au_yaitaka_eswatini_itengue_marufuku_ya_vyama_vya_siasa
Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kubatilishwa marufuku ya kuwepo vyama vya siasa nchini eSwatini (swaziland), sanjari na kuruhusiwa wagombea wa vyama hivyo kuwa na uhuru wa kufanya kampeni za kisiasa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 23, 2018 07:54 UTC
  • AU yaitaka eSwatini itengue marufuku ya vyama vya siasa

Umoja wa Afrika umetoa mwito wa kubatilishwa marufuku ya kuwepo vyama vya siasa nchini eSwatini (swaziland), sanjari na kuruhusiwa wagombea wa vyama hivyo kuwa na uhuru wa kufanya kampeni za kisiasa.

Taarifa ya AU imetolewa siku moja baada ya kufanyika uchaguzi wa bunge katika nchi hiyo ndogo ya Kiafrika.

James Michel, mkuu wa timu ya uangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, AU inauasa utawala wa eSwatini kuangalia upya dikrii ya mwaka 1973 iliyopiga marufuku uwepo wa vyama vya kisiasa katika nchi hiyo ya kifalme.

Aghalabu ya wagombeaji wa viti vya ubunge katika uchaguzi uliofanyika Ijumaa nchini humo ni wapambe wa Mfalme Mswati, ingawaje hawana sauti, kwani kauli ya mwisho na maamuzi yote muhimu nchini humo hutolewa na mfalme huyo mwenye wake 14 na watoto zaidi ya 25.

Mfalme Mswati III wa eSwatini (Swaziland) iliyopata uhuru 1968

Matokeo ya uchaguzi huo hayajatangazwa kufikia sasa. Bunge la nchi hiyo ndilo lenye mamlaka ya kumteua Waziri Mkuu mpya.

Aprili mwaka huu, Mfalme Mswati III wa Swaziland alibadili jina la nchi hiyo na kuwa eSwatini kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 50 wa kukomeshwa ukoloni wa Uingereza nchini humo, akisisitiza kuwa, mabadiliko hayo yatapelekea nchi yake irejee katika jina lake asili kabla ya zama za ukoloni wa Muingereza.