Algeria yapokea wakimbizi wa Syria, Libya na Mali
Gazeti moja linalochapishwa nchini Uingereza limeripoti kuwa Algeria imekuwa mwenyeji wa makumi ya maelfu ya wakimbizi kutoka Syria, Libya na Mali.
Tovuti ya habari ya gazeti la al Arab linalochapishwa mjini London Uingereza imeandika kuwa zaidi ya wakimbizi elfu 30 ambao wengi wao wamezikimbia nchi zao kutokana na vita vya ndani katika nchi hizo, hivi sasa wanaishi nchini Algeria, ambapo nusu ya wakimbizi hao ni kutoka Mali, na waliosalia wanatoka Syria na Libya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi ya Mali imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara licha ya nchi hiyo kuungwa mkono na nchi za Ulaya na khususan Ufaransa.
Wakimbizi kutoka Syria pia hivi sasa wamepewa makazi katika miji 22 ya Algeria huku idadi kubwa ya raia hao ikiishi katika miji mikubwa kama ule wa Anaba mashariki mwa nchi hiyo na wa Wahran magharibi mwa nchi, na katika mji mkuu Algiers.
Wakimbizi wa Libya ambao wamelazimika kuzihama nyumba zao na kukimbilia Algeria kwa ajili ya hifadhi kufuatia kujiri vita vya ndani nchini humo baada ya mapinduzi ya Wananchi ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani dikteta Muammar Gaddafi wanakaribia elfu tano.