Marekani inaendelea kuongeza wanajeshi wake barani Afrika
(last modified Tue, 24 Apr 2018 03:17:45 GMT )
Apr 24, 2018 03:17 UTC
  • Marekani inaendelea kuongeza wanajeshi wake barani Afrika

Jeshi la Marekani linajenga kituo cha ndege za kivita zisizo na rubani nchini Niger kwa lengo la kukabiliana na kile wakuu wa Washington wanadai ni 'makundi ya kigaidi' barani Afrika.

Shirika la Habari la Associated Press limechapisha ripoti Jumanne na kusema Jeshi la Anga la Marekani linajenga kituo cha ndege zisizo na rubani za kijeshi (drone) na kwamba kituo hicho kitakamilika na kuanza kutumika Aprili 2019.

Imedaiwa kuwa kituo hicho kimejengwa kufuatia ombi la serikali ya Niger na kwamba kitakuwa karibu na mji wa Agadez ambapo wakaazi wake wengi ni wa kabila la Tuareg.

Inatazamiwa kuwa kituo hicho kitaweza kutumia drone kubwa za kijeshi aina ya MQ-9 Reaper ambazo hivi sasa zinatumia uwanja na ndege wa mji mkuu wa Niger, Niamey.

Kabla ya kuuawa wanajeshi wanne wa Marekani katika hujuma ya kuvizia nchini Niger mwezi Oktoba mwaka jana, hakukuwa na habari rasmi za kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Niger. Hujuma hiyo ilidaiwa kutekelezwa na wanamgambo wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS.

Hivi karibuni Marekani ilitangaza kuongeza idadi ya askari wake nchini Niger kutoka 100 hadi 800. Hadi sasa Marekani haijatangaza ni drone ngapi au idadi ya wanajeshi wake wataokaohudumu katika kituo hicho cha Agadez. 

Tags