Polisi Tanzania yaimarisha usalama kuhusu maandamano, nayo Chadema yayakana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43634-polisi_tanzania_yaimarisha_usalama_kuhusu_maandamano_nayo_chadema_yayakana
Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeimarisha usalama kila kona ya nchi, kutokana na tetesi za kufanyika maandamano ya kesho tarehe 26 Aprili na ambayo yamekuwa yakihimizwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kupinga serikali ya Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2018 09:52 UTC
  • Polisi Tanzania yaimarisha usalama kuhusu maandamano, nayo Chadema yayakana

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeimarisha usalama kila kona ya nchi, kutokana na tetesi za kufanyika maandamano ya kesho tarehe 26 Aprili na ambayo yamekuwa yakihimizwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kupinga serikali ya Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo.

Kufuatia hali hiyo polisi imewataka wananchi wote kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwa kuwa maandamano yanayozungumzwa hayapo na kwamba ni batili. Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kaimu kamanda wa Polisi Kanda Maalum, ACP Sweethbert Njwele amesema jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha kila mtu anafanya shughuli zake kama kawaida bila kuvunja amani hapo kesho.

Maandamano ya wapinzani nchini Tanzania

Hayo yanajiri katika hali ambayo, mapema jana serikali ya Uingereza iliwaonya raia wake wanaoishi Tanzania kuhusiana na maandamano hayo tarajiwa. "Niwahakikishie, jeshi la polisi tumejipanga hakuna maandamano yatakayofanyika hivyo kila mtu aendelee na shughuli zake kama kawaida." amesema Njwele. Akizaungumza na shirikisho la waendesha pikipiki maarufu kama 'bodaboda' jijini Dar es Salaam kwa upande wake msemaji wa shirikisho la  waendesha pikipiki Adamu Kyando amesema: "Kuna taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikihamasisha bodaboda kushiriki maandamano taarifa hizi si za kweli na ni batili."

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Hayo yanajiri katika hali ambayo Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Idrissa Jumbe Mkila, amesema chama hicho hakihusiki na maandamano yoyote yanayotarajiwa kufanyika kesho. Mkila ameyasema hayo leo Aprili 25 wakati akizungumza na waaandishi wa habari katika ufunguzi wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo viongozi wa chama Wilaya na Mikoa huko Kikwajuni Mkoa Mjini Unguja. Ni muda sasa ambapo kumekuwepo kauli kuhusiana na maandamano tarajiwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii chini Tanzania suala ambalo limelifanya jeshi la polisi nchini humo kuchukua tahadhari.