Tanzania yaadhimisha miaka 54 ya muungano, wapinzani waitisha maandamano
Tanzania leo inaadhimisha miaka 54 tangu Tanganyika na Zanzibar zilipoungana na kuunda taifa moja la Tanzania huku baadhi ya wapinzani wakiitisha maandamano ya kuipinga serikali.
Tarehe 26 Aprili 1964, Tanganyika iliugana na Zanzibar na kuunda serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na Rais John Pombe Magufuli mjini Dodoma, na yanafanyika huku nchi hiyo ikiendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limeimarisha usalama kila kona ya nchi, kutokana na tetesi za kufanyika maandamano leo ambayo yamekuwa yakihimizwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya kupinga serikali ya Rais John Pombe Magufuli.
Hata hivyo kunaonekana kuwepo mgawanyiko mkubwa miongoni mwa wapinzani baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, Idrissa Jumbe Mkila, kusema chama hicho hakihusiki na maandamano yoyote yanayotarajiwa kufanyika leo.
Mwanaharakati wa kwenye mitandao ya kijamii, Mtanzania anayeishi Marekani Mange Kimambi amekua akiratibu maandamano kupitia ukurasa wake wa Instagram, akiitisha maandamano nchi nzima dhidi ya Rais Magufuli kwa kile anachodai kuwa amekuwa akikiuka haki za binaadamu na kukandamiza uhuru wa kisiasa nchini Tanzania.