May 08, 2018 07:39 UTC
  • Watu 1000 waliokuwa wametekwa na Boko Haram Nigeria waokolewa

Jeshi la Nigeria limesema hivi karibuni lilifanikiwa kuwaokoa mateka wapatao elfu 1 kutoka kwa kundi lenye msimamo mkali la Boko Haram katika jimbo la Borno.

Msemaji wa jeshi la Nigeria Bw. Texas Chukwu amesema, operesheni za kuwakomboa mateka hao zilifanywa kwa ushirikiano na majeshi ya Cameroon, Chad na Niger.

Mwezi Aprili pia Jeshi la Nigeria lilitangaza kuwa, limewakomboa mateka 149 kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Mwezi Machi  kundi hilo la kigaidi la Boko Haram liliwaachia huru mabinti 100 kati ya 110 liliowateka nyara mwezi Februari mwaka huu, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Magaidi wa Boko Haram

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wameshapoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags