Tanzania: Hakuna ugonjwa wa Ebola nchini, lakini tunachukua tahadhari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i44326-tanzania_hakuna_ugonjwa_wa_ebola_nchini_lakini_tunachukua_tahadhari
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, hadi sasa hakuna mtu yeyote nchini aliyegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa wa Ebola, lakini itaendelea kudhibiti na kujikinga na ugonjwa huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2018 03:06 UTC
  • Tanzania: Hakuna ugonjwa wa Ebola nchini, lakini tunachukua tahadhari

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, hadi sasa hakuna mtu yeyote nchini aliyegundulika kuwa na viashiria vya ugonjwa wa Ebola, lakini itaendelea kudhibiti na kujikinga na ugonjwa huo.

Sambamba na hayo, Tanzania imeanza kutekeleza hatua madhubuti za kufuatilia uwezekano wa kesi za ugonjwa huo katika vituo vya mpakani vikiwemo viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari katika mikoa inayopakana na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DR) ambako ugonjwa huo umeripotiwa.

Baadhi ya hatua za kuwastiri watu waliofariki dunia kwa maradhi hayo hatari ambapo hawatakiwi kuguswa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vituo muhimu vya mpakani kati ya nchi hiyo na Kongo DR ni pamoja na Rusumo, Kabanga, Mtukula na Bandari ya mkoa wa Kigoma. Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, juu ya taarifa za ugonjwa huo nchini Tanzania hasa baada ya kuripotiwa kuibuka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kisha kutangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), amesema kuwa serikali inachukua hatua kali kutokana na Tanzania kupakana na Congo. “Taarifa ya WHO ya Mei 8, inaeleza kuwa vipimo vya maabara vimethibitisha baada ya kupokea wagonjwa 21, kati yao 17 wameshapoteza maisha.

Ramani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

"Watu wanaoishi katika mikoa inayopakana na DRC wanapaswa kuchukua tahadhari pale wanapohisi kupata magonjwa yenye dalili za Ebola kwa kuwahi kufika kwenye hospitali na vituo vya afya ili wafanyiwe vipimo vya kina kuonyesha kama wameathirika au la,” alisema Waziri Mwalimu. Waziri wa Afya wa Tanzania aliitaja mikoa ambayo inatakiwa kuchukua tahadhari kuwa ni Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. “Nimeitaja mikoa hiyo kwa sababu ina njia nyingi ambazo siyo rasmi zinazowawezesha watu kuvuka kutoka nchi moja kwenda nyingine na hivyo kusambaa kwa ugonjwa huo kunaweza kuwa rahisi katika mikoa hiyo.”