UN: Wakimbizi 15,000 kutoka Sudan Kusini, DRC wameingia Uganda Aprili
Ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR imebainisha kuwa, wakimbizi 15,000 hususan kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini wameingia nchini Uganda mwezi uliopita pekee wa Aprili.
Kwa mujibu wa shirika hilo, Uganda ambayo hupokea wahajiri zaidi ya 300 kila siku kwa sasa ina takriban wakimbizi milioni moja na laki tano baada ya kusajiliwa wakimbizi hao wapya.
Ruhakana Rugunda, Waziri Mkuu wa Uganda amesema nchi hiyo ya Afrika Mashariki inafanya juu chini kuhakikisha kuwa wakimbizi hao wanajihisi wapo nyumbani na wanapata mahitaji yao ya msingi.
Takwimu zinaonesha kuwa, wakimbizi zaidi ya milioni moja walioko Uganda ni raia wa Sudan Kusini, 276,570 wa Kongo DR, 40,497 kutoka Burundi, 37,193 kutoka Somalia na maelfu ya wengine wanatoka katika nchi za Rwanda, Eritrea na Ethiopia.
Uganda inashuhudia wimbi hilo la wakimbizi katika hali ambayo, mwezi uliopita, Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu liliripoti kuwa, msongamano mkubwa katika hospitali na hali mbaya katika kambi za wakimbizi zimechochea zaidi ugonjwa wa kipindupindu ulioanza mwezi Februari mwaka huu, ambao umeua makumi ya wakimbizi hao.
Kwa mujibu wa shirika hilo, wakimbizi zaidi ya 70 elfu wa DRC wamewasili nchini Uganda tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa na kwamba asilimia 80 miongoni mwao ni wanawake na watoto.