Morocco yaelekeza tuhuma zake kwa Algeria kwamba inaiunga mkono Polisario
Kwa mara nyingine serikali ya Morocco kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imeinyooshea kidole cha lawama serikali ya Algeria kwamba inaiunga mkono harakati ya Polisario, hasa katika kuendesha maneva ya kijeshi na wapiganaji wa harakati hiyo katika eneo Sahara Magharibi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Morocco imeituhumu Algeria kwamba imeshirikiana na harakati hiyo na kwamba maneva yaliyoendeshwa na wapiganaji wa Polisario wa Sahara Magharibi, ni hatua ya uchochezi na ambayo itaweza kuwasha moto katika eneo. Jumapili iliyopita, wapiganaji wa mrengo wa Polisario walifanya maneva katika eneo la Tifariti, moja ya maeneo ya jangwa la nchi hiyo. Ni miaka kadhaa sasa ambapo Morocco imekuwa ikiituhumu serikali ya Algeria kwamba inaiunga mkono harakati hiyo na ni kwa ajili hiyo ndio maana mahusiano ya nchi mbili yakaingia doa.
Eneo la Sahara Magharibi lilikuwa likikoloniwa na Uhispania ambapo mwaka 1975 liliunganishwa na Morocco. Hata hivyo wapiganai wa mrengo wa Ukombozi wa Polisario, wanataka kujitenga eneo hilo. Mapigano kati ya pande mbili za Morocco na Polisario yalianza tangu mwaka 1975 na baada ya hapo mwaka 1991 pande mbili zilitiliana saini ya usitishaji mapigano chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Hivi karibuni pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alizitaka pande mbili kustahamiliana na kujiepusha na jambo lolote linaloweza kuzusha machafuko katika eneo hilo