Baada ya kuitelekeza Taiwan, Burkina Faso yaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China
(last modified Sat, 26 May 2018 15:24:42 GMT )
May 26, 2018 15:24 UTC
  • Baada ya kuitelekeza Taiwan, Burkina Faso yaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China

China na Burkina Faso zimeanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuvunja uhusiano wake na Taiwan, ukiwa ni ushindi mwingine kwa Beijing inayoendelea kutoa mashinikizo kwa serikali ya Taipei.

Hati ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili imesainiwa mbele ya waandishi wa habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi na mwenzake wa Burkina Faso Alpha Barry katika hafla maalumu iliyofanyika leo mjini Beijing.

Kufuatia hatua hiyo, sasa Taiwan imebaki kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi moja tu ya Kiafrika, ambayo ni Jamhuri ya eSwatini (Swaziland). Kwa ujumla kisiwa hicho kwa sasa kina uhusiano na nchi 18 tu duniani, baada ya Jamhuri ya Dominican, Sao Tome and Principe na Panama kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na kisiwa hicho.

Aghalabu ya nchi ambazo zina uhusiano na Taiwan kwa sasa ni nchi maskini hasa za Amerika ya Kati na Pasifiki kama vile Belize na Nauru. China inaitambua Taiwan ambayo mwaka 1949 ilijitenga na nchi hiyo baada ya vita vya ndani, kuwa ni sehemu ya ardhi yake na kwamba haina haki ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na nchi nyingine yoyote ile.

Uhasama wa China kwa Taiwan umeongezeka tangu Tsai Ing-wen kuchaguliwa kuwa rais wa kisiwa hicho katika uchaguzi wa mwaka  2016, kutokana na hofu iliyonayo Beijing kwamba kiongozi huyo ana nia ya kutangaza uhuru rasmi wa kisiwa hicho. Hata hivyo Bi Ing-wen anasisitiza kuwa anataka kuendeleza hali hiyohiyo ya kimamlaka iliyonayo Taiwan hivi sasa.../