May 31, 2018 14:48 UTC
  • Wakenya waandamana kulaani ufisadi wa kifedha serikalini

Mamia ya wananchi wa Kenya wamefanya maandamano hii leo katika mji mkuu Nairobi, kulalamikia kiwango kikubwa cha ufisadi wa fedha nchini humo.

Waandamanaji hao wanasema ni jambo la kusikitisha namna taifa hilo linapoteza mabilioni ya fedha na hakuna ofisa wa ngazi za juu serikali ambaye amewahi kufungwa jela katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kashfa za ufisadi. 

Maandamano hayo yamefanyika siku chache baada ya vyombo vya usalama kuwatia mbaroni makumi ya watu, wanaotuhumiwa kuhusika katika sakata la ufisadi ndani ya Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS), ambapo karibu Shilingi bilioni 9 (dola milioni 100 za Marekani) zilipotea.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema wanaodaiwa kuiba fedha za umma kutoka NYS, wabebe mzigo wao wenyewe na wasimlaumu yeyote

Tayari washukiwa 24 kati ya 54 wamefikishwa mahakamani na kukanusha madai dhidi yao.

Watuhumiwa 24 walioshtakiwa kuhusiana na kashfa hiyo ya ufujaji wa pesa za NYS watakaa rumande kwa wiki moja kabla ya kutolewa uamuzi wa kuachiliwa kwa dahamana.

Miongoni mwa waliopandishwa kizimbani siku ya Jumanne ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana na Jinsia Lilian Mbogo Omollo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la NYS Richard Ndubai.

Tags