Uganda yasisitiza kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amesema kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA ni jambo lenye udharura mkubwa.
Sam Kutesa ameyasema hayo katika mazungumzo na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda Sayyed Morteza Mortazavi. Amesema amesikitishwa sana na kutiwa wasiwasi na hatua ya upande mmoja na ya kinyume cha sheria iliyochukuliwa na Marekani ya kujitoa kwenye makubaliano hayo na kutanabahisha kwamba hatua hiyo itakuwa na athari mbaya na matokeo hasi mengi.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amesema, ana matumaini kwamba pande nyingine zilizosaini makubaliano ya JCPOA yataendelea kuheshimu na kufungamana na makubaliano hayo ya kimataifa.
Kutesa aidha ametaka kuongezwa kiwango cha ushirikiano kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika nyanja za kiuchumi na kueleza matumaini aliyonayo ya kufanya safari hapa nchini muda si mrefu ujao.
Katika mazungumzo hayo, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Kampala Sayyed Morteza Mortazavi amemkabidhi pia Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ujumbe kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje Mohammad Javad Zarif kuhusu hatua na hali yaliyofikia makubaliano ya JCPOA.
Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza uamuzi wa upande mmoja na ulio kinyume cha sheria wa kuiondoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia na Iran, uamuzi ambao umekabiliwa na ukosoaji na upinzani mkubwa wa nchi nyingi duniani.../