Ethiopia yaafiki kutekeleza makubaliano ya suluhu na Eritrea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45508-ethiopia_yaafiki_kutekeleza_makubaliano_ya_suluhu_na_eritrea
Serikali ya Ethiopia imeafiki kutekeleza makubaliano ya suluhu yaliyofikiwa baina yake na Eritrea kwa lengo la kuhitimisha vita na mapigano ya mpakani kati ya nchi mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2018 22:49 UTC
  • Ethiopia yaafiki kutekeleza makubaliano ya suluhu na Eritrea

Serikali ya Ethiopia imeafiki kutekeleza makubaliano ya suluhu yaliyofikiwa baina yake na Eritrea kwa lengo la kuhitimisha vita na mapigano ya mpakani kati ya nchi mbili.

Taarifa iliyotolewa na muungano wa chama tawala nchini Ethiopia wa EPRDF, mbali na kukubali bila masharti yoyote makubaliano yanayojulikana kama maafikiano ya Algeria imesisitiza kuwa itafanya jitihada kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu, suluhu baina ya Ethiopia na Eritrea inafikiwa na mienendo ya kihasama kati ya nchi mbili inakomeshwa ili kurejesha amani na uthabiti katika eneo.

Kwa mujibu wa hati ya  maafikiano ya suluhu ya Algeria yaliyosainiwa na nchi mbili mwaka 2000, Ethiopia itairejeshea Eritrea maeneo yanayozozaniwa kikiwemo kitongoji cha Badme kwa mujibu wa mpaka mpya wa pamoja ulioainishwa.

Hitilafu na ugomvi wa mpaka uliozuka mwaka 1998 kati ya Ethiopia na Eritrea ulipelekea kuzuka vita vikali vya umwagaji mkubwa wa damu  vilivyoendelea kwa muda wa miaka miwili na kusababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa.

Mahakama ya The Hague ilitangaza wakati huo kwamba Eritrea imekiuka sheria za kimataifa na kuanzisha vita kwa kuishambulia Ethiopia.

Vita hivyo vilimalizika kwa Ethiopia kuyadhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakizozaniwa na pande mbili, lakini baada ya Umoja wa Mataifa kuunda kamati ya kuainisha mpaka wa pamoja wa nchi mbili, mnamo mwaka 2015 iliamuliwa kuwa kitongoji cha Badme kitaunganishwa na ardhi ya Eritrea.../