Jun 09, 2018 08:05 UTC
  • Askari 5 wa Marekani wauawa na kujeruhiwa na al-Shabaab Somalia

Askari mmoja wa Marekani ameuawa huku wengine wanne wakijeruhiwa katika operesheni ya pamoja ya vikosi vya US na askari wa Umoja wa Afrika dhidi ya ngome ya wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia.

Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (Africom) imeripoti kuwa, operesheni hiyo ya jana Ijumaa katika eneo la Jubaland, yapata kilomita 350 kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu, iliwaleta pamoja makumi ya askari wa Marekani na wanajeshi 800 wa Somalia na Kenya KDF wanaohudumu chini ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom).

Aidha askari mmoja wa Somalia alijeruhiwa vibaya baada ya vikosi hivyo vya Marekani na Amisom kushambuliwa kwa maroketi ya wanachama wa al-Shabaab. 

Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga yanayofanywa na ndege zake zisizo na rubani 'drone' nchini Somalia mnamo Juni 2011, lakini hujuma hizo zimeshindwa kulitokemeza kundi hilo la ukufurushaji.

Ramani ya Somalia

Mwaka jana Rais Donald Trump aliidhinisha kutumwa makumi ya askari wa Marekani nchini Somalia, idadi kubwa kuwahi kutumwa na US katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, tangu mwaka 1993.

Itakumbukwa kuwa, Marekani iliviondoa vikosi vyake nchini Somalia mwaka 1993, baada ya wanajeshi wake wasiopungua 18 kudhalilishwa kwa kuuawa na kisha miili yao kuburutwa ardhini katika mji mkuu Mogadishu.

Tags