Magendo ya silaha na ukatili vyashamiri Nigeria
Ongezeko la uuzaji wa silaha kinyume cha sheria nchini Nigeria umezidisha hali mbaya ya kiusalama, ukatili na machafuko katika nchi hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika.
Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Boko Haram ambao mashambulizi yao yamesababisha mauaji ya watu waziopungua elfu 20 huko kaskazini mashariki mwa Nigeria wamekuwa wakiingiza silaha nchini humo kwa njia za magendo kupitia kaskazini mwa Afrika hususan nchini Libya.
Ripoti zinazema silaha hizo ambazo zimepigwa marufu nchini Nigeria, katika miezi ya hivi karibuni zimekuwa zikitumiwa katika mapigano baina ya wafugaji na wakulima huko katikati mwa nchi hiyo.
Tathmini iliyotolewa na taasisi ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, kwa sasa kuna zaidi ya silaha nzito na nyepesi milioni 350 nchini Nigeria.
Jeshi la Nigeria limekuwa likikamata shehena za silaha za aina mbalimbali lakini mpaka wenye urefu wa karibu kilomita 4,000 wa nchi hiyo na nchi jirani umeifanya nchi hiyo ikabiliwe na changamoto kubwa katika kukabiliana na tatizo la uuzaji wa silaha kwa njia za magendo.