Shambulizi la guruneti lajeruhi 9 katika Chuo Kikuu Ethiopia
Watu tisa wamejeuhiwa katika shambulizi la guruneti dhidi ya Chuo Kikuu kimoja kusini mwa Ethiopia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, mtu mmoja aliyekuwa amejizatiti kwa silaha alirusha guruneti ndani ya maktaba ya Chuo Kikuu cha Dilla, katika eneo la Gadua kusini mwa Ethiopia.
Hata hivyo mkurugenzi wa chuo hicho amesema wanachuo waliojeruhiwa hawapo katika hali mbaya sana.
Maafisa usalama nchini Ethiopia wamesema wameanzisha uchunguzi kuwasaka wahusika wa shambulizi hilo huku polisi ikisema haijafahamu kiini hasa cha hujuma hiyo kufikia sasa.
Aprili mwaka huu, watu watatu waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililotokea katika eneo la Oromia, kusini mwa Ethiopia.