Wanamgambo washambulia taasisi za mafuta mashariki mwa Libya
Afisa mmoja wa jeshi la Libya amesema, wanamgambo wenye silaha wameshambulia taasisi za mafuta zilizoko chini ya Jenerali Khalifa Haftar mashariki mwa nchi hiyo na kuchoma moto kwa uchache tangi moja la mafuta.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, shambulio hilo limefanywa na kundi linalojiita "Brigedia za Ulinzi wa Benghazi" ambalo kimsingi linaundwa na watu ambao walifukuzwa mjini Benghazi na vikosi vya Khalifa Haftar katika miaka ya hivi karibuni.
Msemaji wa Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar amesema kuwa, wanamgambo hao wamefurushwa na kikosi cha anga cha jeshi hilo.
Mwezi Septemba 2016, vikosi vya Khalifa Haftar vilifanikiwa kudhibiti maeneo manne makuu ya mafuta ya nchini Libya yaani Zweitina, Bariqa, Ra's Lanuf na Sidra.
Kimsingi mafuta yote ya Libya yanasafirishwa nje ya nchi kupitia maeneo hayo manne ambayo hivi sasa yako mikononi mwa vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkononi ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati.
Mwezi Machi 2017, Brigedi za Ulinzi wa Benghazi zilidhibiti maeneo mawili ya Ra's Lanuf na Sidra, lakini muda mchache baadaye zilifukuzwa na askari wa Khalifa Haftar.