Watu 10 wafariki dunia katika mapigano ya kikabila kusini mwa Ethiopia
Mkuu wa Ofisi ya Mawasiliano wa Jimbo la 'Eneo la Mataifa ya Kusini' kusini mwa Ethiopia ametangaza habari ya kuuawa watu 10 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila.
Sulaiman Hilu amesema kuwa, mapigano hayo yamejiri kati ya watu wa makabila ya Sidama na Wolaita na kwamba yalianza siku ya Jumanne ya tarehe 12 ya mwezi huu. Hilu ameongeza kuwa, mapigano hayo yametokea katika mji wa Awasa (Hawassa) katikati ya jimbo la 'Eneo la Mataifa ya Kusini' na kwamba mbali na watu 10 kuuawa, watu wengine 89 wamejeruhiwa huku wengine 500 wakilazimika kuwa wakimbizi.
Sulaiman Hilu amesema kuwa katika mapigano hayo nyumba kadhaa zimeharibiwa na mali za raia zimeporwa. Makabila ya Sidama na Wolaita ndiyo makabila makubwa ya kusini mwa Ethiopia ambayo kwa miaka kadhaa yamekuwa yakishambuliana mara kwa mara.
Serikali ya Addis Ababa imetangaza kuwa imechuakua hatua kadhaa kwa ajili ya kurejesha usalama katika mji wa Awasa ambao ni makao makuu ya jimbo la 'Eneo la Mataifa ya Kusini.'