Maandamano ya Waislamu yaendelea Nigeria kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46112-maandamano_ya_waislamu_yaendelea_nigeria_kushinikiza_kuachiliwa_huru_sheikh_zakzaky
Waislamu wa mji wa Kaduna wa kaskazini magharibi mwa Nigeria kwa mara nyingine wamefanya maandamano ya kulaani kuendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2018 22:40 UTC
  • Maandamano ya Waislamu yaendelea Nigeria kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky

Waislamu wa mji wa Kaduna wa kaskazini magharibi mwa Nigeria kwa mara nyingine wamefanya maandamano ya kulaani kuendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria, Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Vyombo vya habari vya Nigeria vimetangaza habari ya kuendelea maandamano ya Waislamu hao jana Jumatano na kuongeza kuwa polisi wa Nigeria wamevamia maandamano hayo na kuwajeruhi Waislamu kadhaa.

Katika miezi kadhaa iliyopita, Kaduna imekuwa ikishuhudia maandamano ya mara kwa mara ya Waislamu wa Nigeria wanaoshinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Sheikh Ibrahim Zakzaky

 

Uvamizi na mashambulizi ya polisi kila yanapofanyika maandamano hayo hupelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa Waislamu kadhaa.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alikamtwa baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya yeye na mke wake mwezi Disemba 2015 wakati jeshi la nchi hiyo lilipovamia Husainia ya Baqiyyatullah mjini Zaria na kuua kwa umati mamia ya Waislamu.

Watoto wa kuzaa wa Sheikh Zakzkay ni miongoni mwa mamia ya Waislamu waliouliwa shahidi na  kujeruhiwa na wanajeshi wa Nigeria katika jinai hiyo.

Hivi sasa miaka miwili na nusu imepita tangu kutokea uvamizi huo lakini serikali ya Nigeria ingali inang'ang'ania kumshikilia korokoroni Sheikh Ibrahim Zakzaky licha ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kutoa amri ya kuachiliwa huru.