LHRC: Kuna njia tatu kuu zitakazofanikisha kupatikana katiba mpya Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46186-lhrc_kuna_njia_tatu_kuu_zitakazofanikisha_kupatikana_katiba_mpya_tanzania
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania kimetoa mapendekezo matatu ambayo kwa mujibu wake yatasaidia kupatikana katiba mpya nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2018 09:27 UTC
  • LHRC: Kuna njia tatu kuu zitakazofanikisha kupatikana katiba mpya Tanzania

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini Tanzania kimetoa mapendekezo matatu ambayo kwa mujibu wake yatasaidia kupatikana katiba mpya nchini humo.

Hayo yameelezwa leo na Dk James Jesse, Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), kiongozi wa timu maalumu ya wataalamu iliyoundwa na kituo hicho kwa ajili ya kufuatilia mkwamo wa mchakato wa Katiba Mpya ambapo pamoja na mambo mengine imezitaja njia hizo kuwa mosi, kuendelea na mchakato huo kuanzia pale ulipoishia, sambamba na kutoa fursa kwa wananchi kupigia kura katiba inayopendekezwa. James Jesse ametaja njia ya pili kuwa ni kuundwa timu ya wataalamu watakaoandaa rasimu nyingine ya katiba ambayo itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya ndiyo ama hapana. Njia ya tatu iliyotajwa na timu hiyo ya LHRC ni kuunda mwafaka wa kitaifa ili makundi yatakayoingia katika bunge maalumu la katiba yawe na dhamira moja ya kuandaa katiba bora kwa maslahi ya taifa.

Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Kwa mujibu wa Jesse, mkwamo katika mchakato wa kwanza wa katiba mpya ulisababishwa na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa nchini Tanzania ikiwemo wapinzani kuamua kususia mchakato huo na kupelekea kuzaliwa Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA. "Mwafaka wa kitaifa unaonekana ungekuwa suluhisho na kupatikana kwa Katiba lakini haukuwepo na ndio maana tunaikumbusha serikali kuhuisha upya mchakato huo," amesema Dk Jesse. Pia amebainisha sababu nyingine iliyosababisha mkwamo huo kuwa ni serikali ya awamu ya tano kusisitiza mara kadhaa kwamba katiba mpya si kipaumbele chake bali maendeleo ya taifa.