Magaidi 7 wa Al Shabab, akiwemo Mtanzania, waangamizwa katika mapigano Somalia
Jeshi la Somalia limewaangamiza magaidi saba wa kundi la kigaidi la Al Shabab katika mapigano yaliyojiri katika eneo la Lower Juba kusini mwa nchi hiyo.
Afisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Somalia Abdi Ibrahim Ali amesema miongoni mwa magaidi waliouawa ni gaidi mkufurushaji raia wa Tanzania. Amesema magaidi hao waliouawa katika oparesheni hiyo na wanajeshi wa serikali walikuwa wamechukua udhibiti wa Daraja la Arare kaskazini mwa mji wa Kismayo.
Ali amesema ameongeza kuwa Jeshi la Somalia limeimarisha oparesheni za kuwatimua magaidi waliokuwa wameliteka eneo la Arare na kutumia daraja la eneo hilo kuwalazimu wakaazi kulipa kodi. Hali kadhalika amedokeza kuwa kamanda wa ngazi za juu wa al Shabab ni miongoni wa magaidi waliouawa katika oparesheni hiyo.
Afisa huyo wa Jeshi la Somalia ameongeza kuwa magaidi wawili ni kati ya waliokamatwa katika oparesheni hiyo ya Daraja la Arare lililo kilomita 10 kutoka Jamaane, ngome nyingine ya magaidi hao wa Al Shabab.
Hadi mwaka 2011, magaidi wa al Shabab walikuwa wanadhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya Somalia kabla ya kufurushwa katika miji mikubwa na kubakia kwenye vijiji vya mbali vya nchi hiyo.
Wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika wameshindwa kuwaangamiza kikamilifu magaidi hao na hivi sasa wameongeza mashambulizi yao yanayoathiri pia nchi jirani kama vile Kenya.