Watu tisa wafariki baada ya mripuko wa lori la mafuta Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46428-watu_tisa_wafariki_baada_ya_mripuko_wa_lori_la_mafuta_nigeria
Watu kadhaa wamefariki dunia katika mlipuko wa lori la mafuta uliotokea barabarani jana katika mji wa Lagos nchini Nigeria, na kuchoma magari mengi.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jun 29, 2018 00:13 UTC
  • Watu tisa wafariki baada ya mripuko wa lori la mafuta Nigeria

Watu kadhaa wamefariki dunia katika mlipuko wa lori la mafuta uliotokea barabarani jana katika mji wa Lagos nchini Nigeria, na kuchoma magari mengi.

Lori hilo la mafuta lililipuka wakati lilipopita barabara kuu kati ya Lagos na Ibadan, kusini magharibi mwa Nigeria. Habari zinasema barabara imefungwa, na waokoaji wamekimbilia kwenye eneo la ajali kuzima moto. Mashuhuda wamesema watu wengi walikwama ndani ya magari na kutoweza kutoka kutokana na moto mkubwa.

Maofisa wa mambo ya dharura wamesema mpaka sasa magari takriban 60 yakiwemo mabasi na malori yameteketea katika ajali hiyo, na kazi ya uokoaji bado inaendelea.

Msemaji wa Idara ya Usalama Barabarani Nigerioa, Bisi Kazeem amesema ajali hiyo imejiri karibu na daraja la Otedola katika sehemu ya barabara ya kuondoka Lagos. Amesema sababu ya ajali hiyo ni kufeli breki za lori.

Ikumbukwe kuwa Juni mwaka 2015 karibu watu 70 walifariki huko mashariki mwa Nigeria mjini Onitsha baada ya lori la kubeba mafuta kushika moto. Miaka mitatu kabla pia ajali mbaya sana ya moto wa mafuta iliwaua zaidi ya watu 100 huko Niger Delta katika mkasa uliochangiwa na watu kuchota mafuta yaliomwagika baada ya gari kubwa la mafuta kupata ajali.