Mapatano ya usitishaji vita Sudan Kusini yakiukwa masaa machache baada ya kuidhinishwa
Mapatano ya hivi karibuni ya usitishaji vita Sudan Kusini yamekiukwa masaa machache baada ya kuanza kutekelezwa huku pande zote mbili za serikali na upinzani zikirushiana lawama.
Msemaji wa upinzani Lam Paul Gabriel amesema wanajeshi wa serikali wakishirikiana na waasi kutoka nchi jirani ya Sudan wamefanya hujuma ya pamoja katika eneo la Mboro, Kaunti ya Wau mapema leo asubuhi. Gabriel ametoa wito kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wasimamizi wa usitishaji vita wachunguze tukio hilo na kuongeza kuwa wana haki ya kujilinda. Amesema yamkini Rais Salva Kiir hana udhibiti kamili wa wanajeshi wake au hataki amani.
Katika upande wa pili msemaji wa serikali ya Juba, Ateny Wek Ateny amesema wapinzani ndio walioanzisha mashambulizi. Ameongeza kuwa wapinzani hawana uongozi imara wa kuwadhibiti wapiganaji huku akisema watu wa Sudan Kusini sasa wanapaswa kupewa fursa ya kuwa na amani.
Mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa yaani Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani, Riek Machar kwa ajili ya kufikia mapatano ya kusitisha vita na kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalianza Jumanne iliyopita katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum chini ya upatanishi wa Rais wa Sudan, Omar al Bashir. Pande hasimu siliafiki Jumatano kuhusu usitishaji vita wa kudumu lakini kuna wasi wasi kuwa mapatano haya mapya sawa kadhaa ya huko nyuma yatasambaratika.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kutokana na mashinikizo na ushawishi wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Nchi hiyo changa zaidi duniani ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la kupindua serikali yake.