AU: Wakati wa kuchukua hatua Sudan Kusini umewadia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46488-au_wakati_wa_kuchukua_hatua_sudan_kusini_umewadia
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema wakati umefika wa kuwachukulia hatua wahusika wanaochochea mgogoro nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2018 02:46 UTC
  • AU: Wakati wa kuchukua hatua Sudan Kusini umewadia

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema wakati umefika wa kuwachukulia hatua wahusika wanaochochea mgogoro nchini Sudan Kusini.

Moussa Faki Mahamat amesema hali katika nchi hiyo ni ya kutisha na hilo limechangiwa na kutowachukulia hatua shakshia wanaokiuka makubaliano ya amani katika nchi hiyo mara kwa mara.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkutano wa umoja huo mjini Nouakchott nchini Mauritania na kufafanua kuwa, "Tunatuma ujumbe ulio wazi kabisa kwa wale wamezoea kuvunja makubaliano ya amani ya Sudan Kusini, siku chache zilizopita tulidhani mambo yametengamaa katika nchi hiyo, lakini hivi sasa hali ni ya atiati tena."

Haya yanajiri baada ya mapatano ya hivi karibuni ya usitishaji vita nchini Sudan Kusini kukiukwa, masaa machache baada ya kuanza kutekelezwa huku pande zote mbili za serikali na upinzani zikirushiana lawama.

Salva Kiir (kushoto), Rais Bashir na Riek Machar

Mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa yaani Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani, Riek Machar kwa ajili ya kufikia mapatano ya kusitisha vita na kukomesha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalianza Jumanne iliyopita katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum chini ya upatanishi wa Rais wa Sudan, Omar al Bashir.

Pande hasimu ziliafiki Jumatano kuhusu usitishaji vita wa kudumu lakini kuna wasi wasi kuwa mapatano haya mapya sawa na kadhaa ya huko nyuma yatasambaratika.

Nchi hiyo changa zaidi duniani ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya Kiir kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kuwa alifanya jaribio la kupindua serikali yake.