Algeria yapinga mpango wa Ulaya kuhusu wahajiri haramu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46496-algeria_yapinga_mpango_wa_ulaya_kuhusu_wahajiri_haramu
Waziri Mkuu wa Algeria ametangaza kuwa, nchi yake inapinga mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuanzisha kambi za wahajiri haramu nchini humo.
(last modified 2026-02-25T07:04:48+00:00 )
Jul 01, 2018 13:45 UTC
  • Algeria yapinga mpango wa Ulaya kuhusu wahajiri haramu

Waziri Mkuu wa Algeria ametangaza kuwa, nchi yake inapinga mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuanzisha kambi za wahajiri haramu nchini humo.

Ahmed Ouyahia ambaye anamuwakilisha Rais wa Algeria katika mkutano wa 31 wa viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Nouakchott nchini Mauritania amesema viongozi wa Ulaya wanatafuta eneo la kuanzisha vituo na kambi za kupokea wahajiri haramu na kwamba nchi yake haitakubali suala hilo.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Abdelkader Messahel alikuwa amesisitiza kuwa, nchi hiyo haitatenga eneo lolote kwa ajili ya wahajiri haramu. 

Messahel amesema kuwa, Algeria itapokea wahajiri kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa na nchi jirani na si vinginevyo. 

Viongozi wa nchi za Ulaya siku kadhaa zilizopita na baada ya mazungumzo ya muda mrefu, walikubaliana kuanzisha kambi za kupokea wakimbizi na wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterrania.

Miongoni mwa nukta muhimu za makubaliano ya viongozi wa Ulaya kuhusu wakimbizi ni kutoruhusu tena wimbi la wahajiri kama lile la mwaka 2015 kuelekea katika nchi za bara hilo na kuzidisha operesheni za kupambana na magenge ya kutorosha wanadamu kupitia Libya au nchi nyingine.