IOM: Zaidi ya wahajiri 1000 wamekufa mwaka huu katika Bahari ya Mediterania
Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limetangaza kuwa, zaidi ya wahajiri 1000 wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania tangu ulipoanza mwaka huu wa 2018.
Taarifa hiyo ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) imeeleza kuwa, wahajiri hao wamekufa maji wakiwa katika juhudi za kuelekea barani Ulaya kutokea Libya.
Othman Belbeisi, Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) nchini Libya amesema kuwa, idadi ya wahajiri wanaopoteza maisha katika pwani ya nchi hiyo imeongezeka kwa kiwango cha kutisha.
Baadhi ya ripoti zinaeleza kuwa, hatua za ukandamizaji za Umoja wa Ulaya dhidi ya wahajiri katika siku za hivi karibuni zimepelekea kuongezeka idadi ya wahajiri wanaopoteza maisha.
Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni viongozi wa nchi za Ulaya walikubaliana kuwahamishia kaskazini mwa Afrika wakimbizi na wahajiri haramu wanaoelekea barani Ulaya kupitia bahari ya Mediterania.
Hata hivyo nchi tano za kaskazini mwa Afrika zimekataa mapendekezo ya viongozi wa Ulaya ya kuanzisha kambi maalumu za wahajiri katika ardhi za nchi hizo kwa ajili ya kuwapokea wahajiri wa Kiafrika.
Licha ya kuwa, idadi ya wakimbizi wanaoelekea Ulaya imepungua kwa kiasi fulani, lakini bado maelfu ya wahajiri na wakimbizi wanapanda mawimbi ya bahari ya Mediterrania kuelekea barani humo lengo likiwa ni kwenda kutafuta maisha mazuri.