Ethiopia yayaondoa makundi 3 ya kisiasa katika orodha ya 'magaidi'
Serikali ya Ethiopia imeyaondoa makundi matatu ya upinzani katika orodha ya 'makundi ya kigaidi', huo ukiwa ni muendelezo wa hatua za mageuzi zinazochukuliwa na Waziri Mkuu wa sasa, Abiy Ahmed.
Kanali ya televisheni ya serikali Fana Broadcasting Corporation imetangaza kuwa, bunge la nchi hiyo leo Alkhamisi limepasisha kwa kishindo sheria inayotaka kuondolewa makundi hayo ya kisiasa katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Makundi hayo ni pamoja na Ogaden National Liberation Front na 'Ginbot 7'.
Hii ni katika hali ambayo, mapema leo, shirika la Kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake mpya kuwa, maafisa wa usalama nchini Ethiopia wamewatesa na kuwabaka wafungwa wa kisiasa wa vuguvugu linalopigania kujitenga la Ogaden National Liberation Front katika jela ya siri iliyoko katika Jimbo la Somali, kati ya mwaka 2011 na mwaka huu.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo amekiri kuwa maafisa wa usalama wamewatesa raia, na sasa mashinikizo ya kutaka kuchukuliwa hatua maafisa waliohusika na vitendo hivyo yameongezeka.
Kundi la Ginbot 7 ambalo pia limeondolewa katika orodha hiyo ya makundi ya kigaidi mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni, lilitangaza uamuzi wa upande mmoja wa kusimamisha kwa muda usiojulikana operesheni zake zote za utumiaji silaha katika maeneo yote ya nchi.
Lilisema kuwa limechukua hatua hiyo chanya ili kuonyesha uungaji mkono kwa msururu wa mageuzi unaofanywa hivi sasa na chama tawala EPRDF.