Serikali na waasi kuondoa vikosi vyao maeneo ya mijini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46614-serikali_na_waasi_kuondoa_vikosi_vyao_maeneo_ya_mijini_sudan_kusini
Pande hasimu katika mgogoro wa Sudan Kusini zimeafiki pendekezo la kuviondoa vikosi vya wapiganaji wao katika maeneo ya mijini nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 07, 2018 02:37 UTC
  • Serikali na waasi kuondoa vikosi vyao maeneo ya mijini Sudan Kusini

Pande hasimu katika mgogoro wa Sudan Kusini zimeafiki pendekezo la kuviondoa vikosi vya wapiganaji wao katika maeneo ya mijini nchini humo.

Jamal Omar, Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Sudan amesema pande mbili hizo zilitoa taarifa jana Ijumaa ya kukubali mpango huo wa kuwaondoa wanajeshi wao katika maeneo ya mijini, kama sehemu ya kutekeleza makubaliano ya amani yaliyosainiwa hivi karibuni mjini Khartoum.

Naye Al-Dierdiry Ahmed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan amesema pande mbili hizo kadhalika zimekubaliana kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa na kivita haraka iwezekanavyo.

Hii ni katika hali ambayo, Jumapili iliyopita, watu wasiopungua 18 waliuawa katika machafuko mapya yaliyozuka nchini Sudan Kusini, baada ya kukiukwa makubaliano mapya ya amani yaliyosainiwa siku chache zilizopita katika nchi jirani ya Sudan.

Rais Salva Kiir (kushoto), Rais Omar Bashir wa Sudan na Riek Machar

Pande hasimu katika mgogoro wa nchi hiyo zinarushiana lawama juu ya vifo hivyo vya raia wasio na hatia katika jimbo la Upper Nile, kaskazini mashariki mwa nchi.

Juni 27, serikali na waasi nchini humo walikubali kuhusu usitishaji vita wa kudumu baada ya kufanyika mazungumzo kati ya mahasimu wawili wa kisiasa yaani Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake wa zamani, Riek Machar, katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.