Jul 08, 2018 13:32 UTC
  • Askari polisi 9 wauawa katika shambulizi la kigaidi nchini Tunisia

Maafisa tisa wa polisi wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea magharibi mwa Tunisia, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.

Shirika la habari la serikali TAP limeripoti kuwa, askari polisi hao wameuawa mapema leo Jumapili baada ya genge moja la kigaidi kuurushia guruneti msafara wa magari ya maafisa usalama hao, katika mji wa Gar Dimaou eneo la Jendouba.

Habari zaidi zinasema kuwa, polisi hao waliviziwa na kushambuliwa na magaidi hao wakufurishaji wanaoaminika kuwa na mfugamanao na Daesh (ISIS), walipokuwa katika operesheni ya kawaida ya kulinda doria.

Inaarifiwa kuwa, idadi hiyo ya askari polisi waliouawa hii leo ndio kubwa zaidi nchini Tunisia tangu mwaka 2015, baada ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kutekeleza wimbi la mashambulizi ya bomu yaliyoua makumi ya maafisa usalama na watalii.

Maafisa usalama katika mji mkuu wa Tunisia, Tunis

Hujuma ya leo imefanyika katika hali ambayo, mwezi Machi mwaka huu, Ofisi ya Rais wa Tunisia ilitangaza kurefusha muda wa hali ya hatari nchini humo kwa miezi saba mingine. 

Sheria ya hali ya hatari ilianza kutekelezwa nchini Tunisia tarehe 24 Novemba 2015 baada ya kutokea shambulio la kigaidi la Daesh dhidi ya basi moja la askari wa ulinzi wa Rais mjini Tunis, ambapo watu 38 waliuawa wakiwemo maafisa 12 wa polisi. 

Tags