Mkutano wa Kihistoraia wa viongozi wa Ethiopia na Eritrea
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali leo amewasili katika mji mkuu wa nchi jirani ya Eritrea, Asmara na kulakiwa kwa taadhima kubwa na rais wa nchi hiyo Isaias Afwerki katika uwanja wa ndege.
Viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo kuhusu njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kuondoa uhasama wa muda mrefu baina yao. Safari hiyo imekuja mwezi mmoja tu baada ya waziri mkuu wa Ethiopia kukubali mapatano ya amani ambayo yamemaliza uhasama wa mpaka baina ya nchi hizo mbili.
Mwezi jana pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea Osman Saleh alitembelea mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa ajili ya mazungumzo ya amani.
Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993 na kisha kukata uhusiano wa pande mbili na hivyo kupelekea Ethiopia ikose njia ya bahari. Mwaka 1998 kuliibuka vita vikali vya mzozo wa mpakani baina ya nchi hizo mbili ambavyo vilipelekea watu zaidi ya 80,000 kupoteza maisha na malaki kuachwa bila makao.

Mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulizipatanisha pande mbili hizo na kusema eneo la mpakani lililokuwa likizozaniwa ni milki ya Eritrea lakini mapatano hayo ya amani hayakutekelezwa. Hatimaye mwezi jana waziri mkuu wa Ethiopia aliwashangaza wengi alipokubali mapatano hayo ya amani.
Waziri wa Habari wa Eritrea Yemane Meskel amesema mkutano wa viongozi hao wawili ni wa kihistoria na wa kidugu huku akiongeza kuwa hii ni mara ya kwanza kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kutua Asmara baada ya miaka 20.