Ethiopia na Eritrea zakubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46653-ethiopia_na_eritrea_zakubaliana_kurejesha_uhusiano_wa_kidiplomasia
Nchi mbili jirani za Ethiopia na Eritrea zimekubaliana kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili na kufungua ofisi za kibalozi katika miji mikuu ya nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2018 00:17 UTC
  • Ethiopia na Eritrea zakubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia

Nchi mbili jirani za Ethiopia na Eritrea zimekubaliana kurejesha tena uhusiano wa kidiplomasia baina ya pande hizo mbili na kufungua ofisi za kibalozi katika miji mikuu ya nchi hizo.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana katika mazungumzo ya Rais Abiy Ahmed wa Ethiopia na mwenyeji wake, Isaias Afwerki mjini Asmara. 

Mapema mwezi Juni pia serikali ya Ethiopia ilikuwa imetangaza kuwa imeafiki makubaliano ya amani na Eritrea ambayo yalihitimisha mapigano ya mpakani baina ya nchi hizo mbili. 

Chama tawala nchini Ethiopia kimekaribisha makubaliano ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili yanayojulikana kama Mapatano ya Algeria na kimesisitiza udharura wa kutekelezwa kikamilifu, kujenga uhusiano wa amani na Eritrea na kukomesha mienendo ya kihasama baina ya nchi hizo mbili. 

Marais wa Ethiopia na Eritrea

Kwa mujibu wa Mapatano ya Algeria yaliyotiwa saini mwaka 2000, Ethiopia inapaswa kuikabidhi Eritrea maeneo yote yanayogombaniwa likiwemo eneo la mpakani la Badme. 

Mwaka 1998 hitilafu juu ya umiliki wa maeneo ya mpakani baina ya Ethiopia na Eritrea zilizitumbikiza nchi hizo mbili katika vita vya umwagaji damu vya miaka miwili ambavyo vilisababisha mauaji ya maelfu ya raia wa pande mbili. Mwishoni mwa vita hivyo Ethiopia ilidhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakigombaniwa. Hata hivyo kamati iliyoundwa na Umoja wa Mataifa kushughulikia hitilafu hizo ilihukumu kwamba, neo la Badme ni milki ya Eritrea.