IGAD yapongeza kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ethiopia na Eritrea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46677-igad_yapongeza_kuhuishwa_uhusiano_wa_kidiplomasia_kati_ya_ethiopia_na_eritrea
Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo Mashariki mwa Afrika IGAD imepongeza hatua ya nchi mbili jirani za Ethiopia na Eritrea kukubaliana kurejesha tena uhusiano wao kidiplomasia na kufungua ofisi za kibalozi katika miji mikuu ya nchi hizo, baada ya majirani hao kuhasimiana kwa karibu miongo miwili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2018 02:30 UTC
  • IGAD yapongeza kuhuishwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Ethiopia na Eritrea

Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo Mashariki mwa Afrika IGAD imepongeza hatua ya nchi mbili jirani za Ethiopia na Eritrea kukubaliana kurejesha tena uhusiano wao kidiplomasia na kufungua ofisi za kibalozi katika miji mikuu ya nchi hizo, baada ya majirani hao kuhasimiana kwa karibu miongo miwili.

Balozi Mahboub Maalim, Katibu Mkuu wa IGAD sambamba na kumpongeza Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa ujasiri na jitihada zake za kufufua uhusiano wa Addis Ababa na Asmara, amesema "Kuhuishwa uhusiano wa Eritrea na Ethiopia na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa mpaka wa miaka mingi bila shaka kutakuwa na maslahi na manufaa kwa wananchi wa nchi mbili hizo." 

katika ujumbe wake, Mhandisi Mahboub Maalim ameeleza kuwa anatumai Eritrea itajiunga tena na jumuiya ya IGAD huku akisisitiza kuwa, kuhuishwa uhusiano wa nchi mbili hizo za Pembe ya Afrika kutaimarisha amani, uthabiti na utangamano wa kibiashara katika nchi zote za eneo na bara la Afrika kwa ujumla.

Waziri Mkuu wa Ethiopia (kushoto) na Rais wa Eritrea mjini Asmara

Makubaliano hayo ya kufufua uhusiano wa pande mbili yalifikiwa juzi Jumapili katika mazungumzo ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea mjini Asmara.

Mwaka 1998 hitilafu juu ya umiliki wa maeneo ya mpakani baina ya Ethiopia na Eritrea zilizitumbikiza nchi hizo mbili katika vita vya umwagaji damu vya miaka miwili ambavyo vilisababisha mauaji ya maelfu ya raia wa pande mbili. Mwishoni mwa vita hivyo Ethiopia ilidhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakigombaniwa.