Ethiopia kuharakisha utekekezaji mapatano na Eritrea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46688-ethiopia_kuharakisha_utekekezaji_mapatano_na_eritrea
Waziri Mkuu wa Ethiopia leo amesema serikali yake inalenga kutekeleza haraka mapatano yaliyofikiwa na nchi jirani ya Eritrea ili kujaza pengo la fursa zilizopotea katika miongo miwili ya uhasama baina ya nchi hizo mbili jirani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2018 09:21 UTC
  • Ethiopia kuharakisha utekekezaji mapatano na Eritrea

Waziri Mkuu wa Ethiopia leo amesema serikali yake inalenga kutekeleza haraka mapatano yaliyofikiwa na nchi jirani ya Eritrea ili kujaza pengo la fursa zilizopotea katika miongo miwili ya uhasama baina ya nchi hizo mbili jirani.

Siku ya Jumatatu Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alifika katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, na kukutana na rais wa nchi hiyo Isaias Afwerki ambapo pande mbili zilitiliana saini mapatnao ya kumaliza ' hali ya vita' ambayo imekuwepo baina ya nchi hizo mbili kwa miongo miwili sasa.

Katika barua aliyomtumia Isaias Afwerki siku ya Jumanne, Abiy Ahmed amesema serikali yake iko tayari kutekeleza mapatano yaliyofikiwa ili kuwawezesha wananchi wa Ethiopia na Eritrea wapate fursa bora zaidi.

Eritrea ilijitenga  na Ethiopia mwaka 1993  na kisha kukata uhusiano wa pande mbili na hivyo kupelekea Ethiopia ikose njia ya bahari. Mwaka 1998 kuliibuka vita vikali vya mzozo wa mpakani baina ya nchi hizo ambavyo vilipelekea watu zaidi ya 80,000 kupoteza maisha na malaki kuachwa bila makao.

Mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulizipatanisha pande mbili hizo na kusema eneo la mpakani lililokuwa likizozaniwa ni milki ya Eritrea lakini mapatano hayo ya amani hayakutekelezwa. Hatimaye mwezi jana waziri mkuu wa Ethiopia aliwashangaza wengi alipokubali mapatano hayo ya amani.

Mapatano mapya  ya kihistoria baina ya Eritrea na Ethiopia yamepongezwa na nchi za eneo pamoja na jumuiya za kimataifa.